Panapo Moto Hufuka

Dhahiri hudhihirika, lionekalo hubaki,
Mahaba ujapoyataka, ukweli hautengeki,
Ungajitwika faraka, wa papo na mafasiki,
Panapo moto hufuka, ishara hazifichiki.

Fichwalo hugundulika, usiwe huambiliki,
Ongea kutambulika, nyamaza husaidiki,
Lije la Kutatulika, atakufaa rafiki,
Panapo moto hufuka, ishara hazifichiki.

Moshi ndo hutambulika, moto hausitiriki,
Pitapo palipowaka, halikosekani baki,
Kovu haitotibika, kabisa haikutoki,
Panapo moto hufuka, ishara hazifichiki.

Jambo litatatulika, iwapo halibaniki,
Halikosi bainika, faraja au la dhiki,
Lazima litasomeka, iwapo halisemeki,
Panapo moto hufuka, ishara hazifichiki.

Unapokuwa na shaka, kwetu halifunikiki,
Maovu yakikushika, sisemi hatuyapati,
Lazima kueleweka, jambo haligubikiki,
Panapo moto hufuka, ishara hazifichiki.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *