Mapenzi Kuyakimbia

Wafungue masikizi, naomba kwako Jalia,
Watambue watambuzi, neno nilo kusudia,
Ni jaza yake mwenyezi, mapenzi katujalia,
Mapenzi kuyakimbia, miye nasema siwezi.

Mapenzi ja usingizi, ukikosa waumia,
Hakuna asoma maizi, ayari kimsikia,
Miye siwi mpuuzi, ni sege kuyakimbia,
Mapenzi kuyakimbia, miye nasema siwezi.

Wayasingayo kutuzi, namba hawakutimia,
Si mwenye hila Azizi, tabuni akatutia,
Hayano kwangu ni ngozi, vipi nitayachukia?
Mapenzi kuyakimbia, miye nasema siwezi.

Hiki chema kitulizi, nafusi ikiumia,
Yanazuia machozi, wala huwezi kulia,
Kwangu mimi kikohozi, sifichi nawaambia,
Mapenzi kuyakimbia miye, nasema swezi.

Penzi lataka mbawaazi, si ubwana na jaria,
Vinginevyo huliwezi, dosari utalitia,
Kwangu limekuwa vazi,hadhiri najivalia,
Mapenzi kuyakimbia, miye nasema siwezi.

Uyaitae tatizi,waidanganya dunia,
Unawafunga maozi, kweli umeikalia,
Mapenzi hayanikwazi, kwa mbizi nimezamia,
Mapenzi kuyakimbia, miye nasema siwezi.

Ni wadiri siongezi, beti zimesha timia,
Mapenzi sio ghamizi, mkisafiana nia,
Si hirizi si mzizi, imi nayakumbatia,
Mapenzi kuyakimbia, miye nasema siwezi.

© Hamisi A.S. Kissamvu
Mabibo, Dar es Salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *