Nionyeshe Pendo Lako

Simi bubu naongea, sababu ningali hai,
Mbinguni napasha dua, ingawa mie sifai,
Nionyeshe pendo lako, ninakuomba Rabuka.

Ninakuomba Rabuka, uliko kule enzini,
Moyoni nina wahaka, ninatamani kanani,
Nionyeshe pendo lako, Wadudi wangu tabibu.

Wadudi wangu tabibu, ninajua mie muwi,
Ni mengi yalinisibu, na kunena hata mawi,
Nionyeshe pendo lako, Rabbi unighofirie.

Rabbi unighofirie, nikupendeze jamani,
Siniache nijutie, na kujona taabani,
Nionyeshe pendo lako, baba Mungu muumbaji.

Baba Mungu muumbaji, nakuomba nisikie,
Sitaki mie mtaji, karo unisaidie,
Nionyeshe pendo lako, unitakie na heri.

Unitakie na heri, nibukuapo mabuku,
Majaribu unibari, sinivute ja sumaku,
Nionyeshe pendo lako, nisiwe na majivuno.

Nisiwe na majivuno, na kudhani nimefika,
Watu kuwapa mkono, nijipate nawepuka,
Nionyeshe pendo lako, usiniache Manani.

© Hosea Namachanja

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *