Huna Hadhi Huna Haki

Hunalo la kujinaki, ila lako kutulia,
Dhiki baada ya dhiki, tena wingi wa udhia
Mwanadamu ku, zidi kujinyamazia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Ukata utakuteka, bila la kufurahia,
Kuyumba na kuudhika, ndilo lako kubakia,
Mateso kutaabika, tena wingi kuumia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Tenda lako likufae, tena iwe njema nia,
Bahati ikatandae, hata kama yafifia,
Tena vema unyamae, wengine kuangazia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Usijione kujua, wengine wajijulia,
Ama la kujifutua, na debe kujipigia,
Chunguza na kutambua, dunia yanotukia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Unasema una mali, makubwa kujitakia,
Itazame yako hali, ujue yakikujia,
Ulijue la ukweli, uwe wajifahamia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Hata ua hunyauka, chini kujiangukia,
Tena hufa wanowika, kuwahusu hufifia,
Dunia hukugeuka, ukabaki kuumia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Usijidai kujua, usijute na kulia,
Ya ulimwengu tambua, ujue yanowadia,
Yalo mafumbo fumbua, kwa mema ukajitia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

© Kĩmani wa Mbogo
Mwanagenzi Mtafiti

Maoni 1

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *