Umesahau Ulikotoka

Kaka umepata mali, kwa wingi umetukuka,
Sasa una ubahili, kuwa umenufaika,
Shausahau usuli, vile ulivyoteseka,
Umesahau asili, nyumbani ulikotoka!

Hujawa nazo fadhili, vema ukaaminika,
Mali yasiyo halali, kwa hayo kabadilika,
Umejawa ukatili, ilikwondoka shabuka,
Umesahau asili, nyumbani ulikotoka!

Tumebaki na maswali, ya vile unavyowika,
Wendako kila mahali, mwinyi unafahamika,
Tena ukaishi mbali, kwako kusikofikika,
Umesahau asili, nyumbani ulikotoka!

Huna jambo la ukweli, liwe la kuaminika,
Wambiwalo hukubali, vema umetambulika,
Umekosa maadili, japo umenawirika,
Umesahau asili, nyumbani ulikotoka!

Tunakuona fidhuli, kwa hizo zako huluka,
Huna la kutajamali, kaka umeimarika,
Sasa umekuwa nduli, mgumu wa kukumbuka,
Umesahau asili, nyumbani ulikotoka!

Ulivyokuwa awali, siha umedhoofika,
Sasa hujali hubali, umezipata baraka,
Umeshakuwa fahali, hunalo la kusumbuka,
Umesahau asili, nyumbani ulikotoka!

Shida ulivyohimili, sasa zimekuondoka,
Huo wako ujahili,kaburi utakuweka,
Hupendi watu dhalili, vile umetimilika,
Umesahau asili, nyumbani ulikotoka!

Kwa hizo zako idili, kilio kitakufika,
Ujionavyo rijali, subiri kufazaika,
Tunazo zetu akili, kutwa moja tutafika,
Umesahau asili, nyumbani ulikotoka!

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *