Yawaje Kinda Alinda?

Yuwaimba za kushinda, sauti iso kifani,
Nyimbo utakazopenda, zijapo masikioni,
Hutazama wanopanda, mnalo fumbo mtini,
Yawaje kinda alinda, kiotani mna nini?

Ana sime tena panda, usalama yu makini,
Hakosi yake ajenda, fumbo tusilothamini,
Ameamua kutenda, yu dhabiti kwa imani,
Yawaje kinda alinda, kiotani mna nini?

Kikwazo amekiunda, utadhani gerezani,
Ndege nina amekwenda, kaselea ugenini,
Fununu zimeshatanda, umeshakuwa uneni,
Yawaje kinda alinda, kiotani mna nini?

Harufu ni ya kuvunda, itokayo humo ndani,
Bidhaa zilizoganda, oza usikotamani,
Jambo la mali kuponda, matumizi ya mapeni,
Yawaje kinda alinda, kiotani mna nini?

Maonesho anadinda, vilivyomo tubaini,
Tujue wanavyowinda, wafanyavyo mawindoni,
Nimesema yote kenda, la kumi usitamani,
Yawaje kinda alinda, kiotani mna nini?

© Kĩmani wa Mbogo
Mwanagenzi Mtafiti

Maoni 2

  1. Abed Anthony

    kazi nzuri ambayo imenijengea taswira thabiti ya maisha ya aina ya lindo, uaminifu na udadisi.

    Jibu

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *