Usifate ya Waongo

Ukweli atakataa, kana kwamba siyo mwongo,
La kweli atapindua, kwazo nyingi zake tungo,
Mwili mwema atavaa, azifanye zake mingo,
Usifate ya waongo, jifunze kusubiria.

Wala sana hatokaa, ‘kitimia lake lengo,
Haraka atakimbia, apotee kwenye jengo,
Achotaka kachukua, kaliacha na mapengo,
Usifate ya waongo, jifunze kusubiria.

Utabaki tu kulia, kwa kushindwa fanya fungo,
Wazi ukamuachia, alipite lako lango,
Wala hukumzuia, asicheze na viungo,
Usifate ya waongo, jifunze kusubiria.

Hapo mwanzo ‘livutia, sasa lageuka pango,
Hakuna wa kuingia, hata ukitoa hongo,
Lachekwa kwa kufulia, na mengi mingi minango,
Usifate ya waongo, jifunze kusubiria.

Ukubwa ‘lijivunia, ulipouvunja ungo,
Ukataka kuujua, ule utamu wa tango,
Kumbe waenda umia, kwa kutojua mpango,
Usifate ya waongo, jifunze kusubiria.

Kwa tabu umejilea, kutwa kucha pinda gongo,
Watu wakakusifia, ukapanda na viwango,
Shetani likikujia, ulete yako maringo,
Usifate ya waongo, jifunze kusubiria.

Nawe kijana sikia, uliyekomaza shingo,
Tabiayo jivunia, ‘metutumbukia nyongo,
Jehamu tutakutia, au tukupige zongo,
Usifate ya waongo, jifunze kusubiria.

Kwa kughani meambaa, kusema tabia fyongo,
Kiwasihi kutulia, msitoke kwenye zingo,
Lilojema we chukua, hata kama kwako dongo,
Usifate ya waongo, jifunze kusubiria.

© Alvin Aron, 2018
Tunevin.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *