Busara za Nyanya

Keti tako n’kurifu, funzo letu la kizazi,
Ari k’zidi sarafu, usitie upuuzi,
Ifungue y’ko sefu, nis’kie ja mzazi,
Us’erereke maweni, yas’chunuke kalio.

Yapo manne yashike, maneno haya dhahabu,
Ni muhimu uyatake, isikukose adabu,
U’spende upotoke, usipatiwe adhabu,
Mwacha mila atumike, kubaki mjalaana.

Heshima nayo muhimu, kwa waja na hayawani,
Ukitaka kuwa sumu, jipambie maovuni,
A’shini pema kudumu, hubidi ‘jitambuleni,
Staha hupa mwangaza, mja ‘asite upovu.

Pendelea kupa staha, sipende mno wakupe,
Wape leo kama jana, usiwatukane kupe,
Asante nawe nena, shukurani isihepe,
Asante neno jepesi, halitozi mja hela.

Ukamwona mwenza mja, akilia kwa msiba,
Us’mhepe akija, uelewe yake tiba,
Geuka yake faraja, tema pole kama saba,
Ubebe wake mzigo, pole neno la dhahabu.

Ukakos’a mtu wako, kumtenda liso zuri,
Tamkia kinywa chako, pendelea kukariri,
Samahani ni ‘upako, hili neno lenye heri,
Uko’sea samahani, hukuwi eti mjinga.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *