Kamaru Pumzika

Machozi ya kimahaba, hudodoka kiuchongo,
Na kilio si haba, maweni na kwenye pango,
Tumempoteza baba, zaumia zetu chango,
Tuliza sasa peponi, Kamaru shujaa wetu.

Nyimbo zako zapendea, nchini na ughaibu,
Nyimbo nazo zalelea, kuongoa hata bubu,
Adabu hujachelea, kukemea masaibu,
Gitaa yako icheze, kupa wako ujagina.

Nakupa neno hayati, we kamaru mwendazake,
Hakika ulizatiti, umetuacha kwa shake,
Kupa sifa ni shariti, ikibidi nijiwike,
Sauti yangu sikike, na yako izidike.

Kukashifu utengano, kutaka utangamano,
Ukaziandika ngano, kung’aa yako maono,
Maneno ya msumeno, kuletea upatano,
Mti mkuu umegwa, ila hatuyumbiyumbi.

Kwa nyimbo ulitabiri, ‘kubiria serikali,
Vimaneno kukariri, kutoboa siri kali,
Kuzua yale ya heri, kujuzia pilipili,
Nyimbo zako zongolewa, kwa mwana ziongolea.

Roho roho pumzika, roho lala salimini,
Ubakie kusifika, miezi na miakani,
Jibana naye tukuka, tubakie kwa imani,
Kamaru we mwendazake, pumzika kwa amani.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *