Salamu Zetu

Shikamoo mwana wangu, ketia ‘pa kigondani,
Nikupe wosia wangu, mafunzo ya hekimani,
Afirika na uzungu, idumie heshima
Keti kufunze salamu, sibakie u haramu.

Hujambo jikumbukie,kirefu ni huna jambo,
Sijambo nijibilie, eti hunacho kijambo,
Heshima iangazie, ipendeze kama wimbo,
Keti kufunze salamu, sibakie u haramu.

Asalamu leikumu, jibie hiyo salamu,
Aleikum salamu, ni lugha ya kisilamu,
Na sasa ni yako zamu, nijibie kwa hamu,
Keti kufunze salamu, sibakie u haramu.

Waambaje kumbukia, maana wasema nini,
Sina la kukuambia, pokea huo uneni,
Jibule kuchagulia, hilo ni lenye thamani,
Keti kufunze salamu, sibakie u haramu.

Sabalikheri semea, haswa kifika subuhi,
Pendelea kujulia, huku uso mefurahi,
Ni dhima kukariria, taadhima uiwahi,
Keti kufunze salamu, sibakie u haramu.

Masalikheri kumbuka, kunisemea jioni,
Neno hilo tambulika, litamkile kinywani,
Si vizuri kutambuka, leo na siku usoni,
Keti kufunze salamu, sibakie u haramu.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *