Urafiki Unafiki

Natokeza wanguwangu, kuyatema maudhia,
Ya moyo haya machungu, nayotaka kukwambia,
Zakereza hizi pingu, kunitia kuumia,
Urafiki panya paka, wadhani si unafiki?

Kumbe ngozi ni kondoo, mle ndani mbwamwitu,
Kitazamia kioo, kumbe we u jini jitu,
Kwenye simu ni ‘haloo, ndugu nifae kwa kitu,
Urafiki panya paka, wadhani si unafiki?

Chako chema utapata, wakificha mfukoni,
Halafu wakipakata, na kingine mikononi,
Kikuomba we wateta, kwamba we huna hunani,
Urafiki panya paka, wadhani si unafiki?

Nikawa karibu nawe, muda wote tabasamu,
Nikiwa mbali na wewe, wabakia kuwa sumu,
Wanifanyia jimwewe, kunitenda ya haramu,
Urafiki panya paka, wadhani si unafiki?

Siri zangu za maisha, yale kale na kisasa,
Yote yote hukupasha, ya kigumba na kitasa,
Mtima na huniwasha, kuvighana vyangu visa,
Urafiki panya paka, wadhani si unafiki?

We mwenza ndumakuwili, mja msi uadamu,
Neelewa yako hali, ni baridi yako damu,
Wakutoka uhalali, kukupata uharamu,
Urafiki panya paka, wadhani si unafiki?

Ningeweza kuchagua, ngechagulia hekima,
Unafiki kubagua, kuondolea lawama,
Na mazuri kutegua, ubakie kuwa mwema,
Urafiki panya paka, wadhani si unafiki?

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *