Nyang’oro Wanichekesha

Ninazituma salamu, kwako Nyang’oro Isaka,
Mimi nipo Dasalamu, ndimi kaka yako Suka,
Si kwamba nakutuhumu, usije kukasirika,
Kifungo ulichofungwa, waama wewe ndo chanzo.

Chuo ulipohitimu, sote tulifarijika,
Unayo sasa ilimu, na shahada umefika,
Ila hata kujikimu, kwako bado patashika,
Kifungo ulichofungwa, waama wewe ndo chanzo.

Umeziandama simu, jembe hutaki kushika,
Waituhumu mizimu, kwamba ndo imekuteka,
Kuonyeka ni mgumu, kijiji kimekuchoka,
Kifungo ulichofungwa, waama wewe ndo chanzo.

Wapuliza mapafyumu, na jasho lilikutoka,
Koti kubwa ja hakimu, na kabegi umeshika,
Huna jambo la muhimu, washinda ukizunguka,
Kifungo ukichofungwa, waama wewe ndo chanzo.

Hutoi japo salamu, kwa watu wakila rika,
Wakubwa huwaheshimu, sio dada wala kaka,
Sasa kwakila sehemu, sifa mbaya wasemeka,
Kifungo ulichofungwa, waama wewe ndo chanzo.

Kwako nimetia timu, nikuonye kwa hakika,
Leo nakutoa sumu, ‘sizidi kutaabika,
Sipendi kukudhulumu, madhila yakakufika,
Kifungo ulichofungwa, waama wewe ndo chanzo.

Mafundisho ya mwalimu, jaribu kuyakumbuka,
Ili ushike hatamu, uliko uweze toka,
Dunia uone tamu, katika mingi miaka,
Kifungo ulichofungwa, waama wewe ndo chanzo.

Nami hapa nahitimu, kaditama nimefika,
Natua chini kalamu, mipaka nisije vuka,
Usiwe mwanaharamu, embu leo badilika,
Kifungo ulichofungwa, waama wewe ndo chanzo.

© Kinyafu MarAcos
Dar es salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *