Dunia

Dunia hebu sikia, haya ninayokwambia,
Umejawa na udhia, hadi wengine wali,
Mazuri watufichia, mabaya waachilia,
Dunia ewe dunia, walee vyema wanangu.

Dunia huna huruma, waviharibu vizazi,
Wawafanyia hujuma, watoto hadi wazazi,
Zimeshatoka kalima, wameshachoka walezi,
Dunia ewe dunia, walee vyema wanagu.

Dunia mti mkavu, usokuwa na matunda,
Umejawa na maovu, kila balaa na inda,
Umewachia makovu, wale waliokupenda,
Dunia ewe dunia, walee vyema wanangu.

Dunia rangi rangile, aso hili ana lile,
Wawapi wetu wavyele, waloupata uwele,
Wameondoka na ndwele, iso na tiba milele,
Dunia ewe dunia, walee vyema wanangu.

Dunia kweli hadaa, na ulimwengu shujaa,
Twapata kila balaa, na twaona si kinyaa,
Hata wanaotambaa, wanaogopa tu njaa,
Dunia ewe dunia, walee vyema wanangu.

Sita nina sitasita, kuongezea sitaki,
Kwa upana umepata, yote niliyoshtaki,
Tuepushie matata, na tupe yaliyo haki,
Dunia ewe dunia, walee vyema wanangu.

© Kiambi Daniel

Maoni 1

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *