Niongoze Wadudi

Uliye wangu Wadudi, muumba wa roho yangu,
Kwako leo ninarudi, usikie taabu zangu,
Kama ni kombo ni rudi, kwani ndiwe Mungu wangu,
Nilinde wangu Wadudi, dhidi ya nafsi yangu.

Chesire ninalo kusudi, kugura taifa langu,
Imenishinda biladi, nafunganya vilo vyangu,
Ila ni nzito fuadi, imeningia tewengu,
Nilinde wangu Wadudi, dhidi ya nafsi yangu.

Ingawa hujitahidi, kuwakwepa dada zangu,
Kwazo inda na inadi, hupenya moyo wangu,
Nikashindwa kubaidi, kutoka yao ukungu,
Nilinde wangu Wadudi, dhidi ya nafsi yangu,

Insi huwaburudi, nikitemavyo Kizungu,
Kama umeme na radi, huwapa kizunguzungu,
Kumbe wangu usitadi, umeniletea majungu,
Nilinde wangu Wadudi, dhidi ya nafsi yangu.

Hukemea ufisadi, katika taifa langu,
Ambao ni itikadi, wao viongozi wangu,
Wamegeuka asadi, wanataka roho yangu,
Nilinde wangu Wadudi, dhidi ya nafsi yangu.

Kila siku hutahidi, kupenda jirani zangu,
Ni amri ya Wadudi, tokea tangu na tangu,
Lakini wapo hasidi, huponda juhudi zangu,
Nilinde wangu Wadudi, dhidi ya nafsi yangu.

Kwako leo nimerudi, nikujuze dhiki zangu,
Ndilo lililo kusudi, katika utungo wangu,
Mambo yangu usanidi, ipoe jasadi yangu,
Nilinde wangu Wadudi, dhidi ya nafsi yangu.

Sina jambo la kuzidi, nimemaliza beti zangu,
Zipo nane kwa idadi, tama ya utungo wangu,
Ni jambo limenibidi, kutoa ujumbe wangu,
Nilinde wangu Wadudi, dhidi ya nafsi yangu.

© Moses Chesire (Sumu ya Waridi)
    Kitale, Kenya 

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *