Huwi Mkata Kutaka

Huwezi kujinasuwa, ulimboni ukatoka,
Nashangaa kutambuwa, mja mwenza akucheka,
Hawajui umetuwa, huenda ukaondoka,
Huwi mkata kutaka, Mungu sababu ajuwa!

Huna changu cha kuliwa, matumbo yamekauka,
Wasubiri cha kupewa, chochote kinacholika,
Huvipati vitumbuwa, uchakurapo kwa taka,
Huwi mkata kutaka, Mungu sababu ajuwa!

Wamekuzidia chawa, ngozi imeshagwajuka,
Wadudu hukuchubuwa, uvimbe umekushika,
Fukara umevamiwa, huna lako la fanaka,
Huwi mkata kutaka, Mungu sababu ajuwa!

Hukosi la kuuguwa, nguo nazo kuchanika,
Nyimbo umeshatungiwa, ndiko kudharaulika,
Shairi umeghaniwa, sana unavyoteseka,
Huwi mkata kutaka, Mungu sababu ajuwa!

Kutenga wameamuwa, maswahibu kutoweka,
Umebaki na ukiwa, usiwe wanufaika,
Hunacho cha kupendewa, chako ukakubalika,
Huwi mkata kutaka, Mungu sababu ajuwa!

Kwa sasa hujajaliwa, siku yako itafika,
Sana umeomba duwa, mizigo umejitwika,
Usubiri la Moliwa, utakopata baraka,
Huwi mkata kutaka, Mungu sababu ajuwa!

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *