Sijaweza…

Sijaweza weupeni, matoni n’nacho kiza,
Sijaweza kiotani, mwenyewe kudunduiza,
Sijaweza ya mitini, naona mauzauza,
Sijaweza sijaweza, ningali kinda mtini!

Sijaweza ya angani, ninangu kumuigiza,
Sijaweza ubawani, kupaa naokoteza,
Sijaweza ya hewani, mbawa zangu kutandaza,
Sijaweza sijaweza, ningali kinda mtini!

Sijaweza kidonani, kudonoa kwashangaza,
Sijawezayao nyuni, hayo kuyapatiliza,
Sijaweza ya kubuni, kiota kutengeneza,
Sijaweza sijaweza, ningali kinda mtini!

Sijaweza makundini, hilo linakoroweza,
Sijaweza kivumbini, nguvu nitajipooza,
Sijaweza kwenda chini, kiotani nagoneza,
Sijaweza sijaweza, ningali kinda mtini!

Sijaweza kujauni, wengine huniuguza,
Sijaweza kuamini, hatima nitajipaza,
Sijaweza ya makini, kibongo chanitatiza,
Sijaweza sijaweza, ningali kinda mtini!

Sijaweza dalihini, udhaifu waniweza,
Sijaweza ya medani, hao watanipuuza,
Sijaweza uwajani, kiholela nitacheza,
Sijaweza sijaweza, ningali kinda mtini!

Sijaweza ulumbini, swifa zangu tapunguza,
Sijaweza ya uneni, wakuu wataniteza,
Sijaweza sautini, nyimbo zangu kutangaza,
Sijaweza sijaweza, ningali kinda mtini!

Sijaweza kubaini, waziwazi kueleza,
Sijaweza mwongozoni, wabuji kuwaongoza,
Sijaweza ya wahuni, wasije kunipumbaza,
Sijaweza sijaweza, ningali kinda mtini!

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *