Msinipe Madhabahu

Nihubiri mchukie, misonyo mnitupie,
Kisa onyo langu mie, lawama zinilemee,
Heri kimya mi nikae, waja nisiwakosee,
Msinipe madhabahu, nimegoma kuhubiri.

Kwa nini mnihadae, mitego mnitegee,
Tegoni niangukie, kwa kejeli mkenue,
Bora nisiwaletee, ubaya unepukie,
Msinipe madhabahu, nimegoma kuhubiri.

Mema niwahutubie, kwenu nikajishaue,
Ya longi mkachimbue, kufanya mniumbue,
Mia kombe nilitoe, wa haramu apotee,
Msinipe madhabahu, nimegoma kuhubiri.

Nafasi msinigee, yalo mana niongee,
Jeuri iwazidie, ubaya ‘sitokomee,
Mtu mwema aambae, kasoro msimwonee,
Msinipe madhabau, nimegoma kuhubiri.

© Alvin Aron, 2018

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *