Niokoe Mola Wangu

Ee Mwenyezi ninusuru, ningali ni ujanani,
Nionyeshe yako nuru, nitoke humu gizani,
Waama nitashukuru, siku zote maishani,
Niokoe Mola wangu.

Naishi kama kunguru, aheri ya hayawani,
Sinao tena uhuru, nateseka mtimani,
Si kwamba ninakufuru, nalonga pasi utani,
Niokoe Mola wangu.

Sisemi kwa kuamuru, nakiri kwako Dayani,
Nahitaji kuwa huru, nisibaki taabani,
Wewe hutozi ushuru, kwako ndipo rehemani,
Niokoe Mola wangu.

© Kinyafu Marcos,2018.
Dar es Salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *