Milima Niachieni

Naipiga parapanda, watu wote sikieni,
Niwatoe njia panda, mnijue kiundani,
Hakuna ninachopenda, kama milima jamani,
Tambarare chukueni, milima niachieni.

Kwanza raha kuipanda, vurugu purukushani,
Moyo fasta hunidunda, kama nimeona jini,
Kilele nikikidanda, miye hoi taabani,
Tambarare chukueni, milima niachieni.

Napandaga kwa kupinda, na sichokagi lakini,
Naugulia ja donda, maumivu siyaoni,
Mpaka zije nishinda, nishafika kileleni,
Tambarare chukueni, milima niachieni.

Nashinda kwenye kitanda, mlima ukiwa ndani,
Siogi heri kuvunda, sizitumii sabuni,
Nazidi leta ununda, sitaki kushuka chini,
Tambarare chukueni, milima niachieni.

Hata peku nitapanda, bila soksi miguuni,
Wala sitaki vurunda, ile ladha asilini,
Ni sawa pata kitinda, nikijichoma mibani,
Tambarare chukueni, milima niachieni.

Milima sijaisanda, ukipanda ina nini,
Japo baridi kuganda, mijasho tele mwilini,
Panda hata zote nyanda, wala hutoona ndani,
Tambarare chukueni, milima niachieni.

Inanitoa udenda, niipitapo njiani,
Natamani kuinyanda, yote niiweke ndani,
Tambarare udananda, aridhi hizo za nini,
Tambarare chukueni, milima niachieni.

Kuna vitu naviunda, nikiwapo milimani,
Sijui alonifunda, ila fundi si utani,
Kanifunda ukamanda, siyo mambo kilaini,
Tambarare chukueni, milima niachieni.

© Alvin Aron, 2018

Maoni 2

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *