Patii

Lo! Pati wa patipati, atafutacho sipati
Pembeni hapitipiti, ila pote katikati
Avimeza vichapati, akiketi kaimati
Patii wa patipati, mbona nyumbani haketi?

Patii na patipati, apepeta pwiti pwiti
Kamuone kijishati, kining’iniza ndo fiti
Na vya kishenzi vishoti, vya leso tena katiti
Patii wa patipati, mbona nyumbani haketi?

Leo mtu hamuiti, asharuka kwenye mati
Viguu japo vijiti, hatovifunika eti
Mwanetu mtanashati, kamwazimeni kasuti
Patii wa patipati, mbona nyumbani haketi?

Viguo vinavyofiti, vyapasuka akiketi
Akachekwa na umati, vitozi vyalenga Pati
Nywele zake nyeusi ti, kupaka rangi hasiti
Patii wa patipati, mbona nyumbani haketi?

Okelo w’Esonga
Malenga Mtafunamiwa

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *