Wasaliti wa Dunia

Nanga natia wino, habari nakupeni
Safari urefu wa kino, ilojaa mapeni
Tope kwenye kisigino, halidhuru magotini
Wasaliti wa dunia, binadamu usiwaamini

Rohoni nina dhiki, nikitizama nyumani
Kidonda natia siki, maumivu ya ilini
Fikra yanipa dhihaki, natamani kongoleni
Wasaliti wa dunia, binadamu usiwaamini

Siri sote twachambua, uhusiano wetu wima
Kwa sala twaamkua, imani dete mesimama
Kanisani twatua, kila siku juu milima
Wasaliti wa dunia, binadamu usiwaamini

Leo hii nagundua, nyuma mwiba menidunga
Ninapigwa na butwaa, kilele nikidanda
Mapacha nilidhania, kumbe umekuwa donda
Wasaliti wa dunia, binadamu usiwaamini

Machozi yanitiririka, Siku hii nikiwaza
Shimo natia kiraka, kitandani nikijilaza
Moyoni nahuzunika, kwa ugumu najikaza
Wasaliti wa dunia, binadamu usiwaamini

Siku hiyo itafika, majibu tutayapata
Matendo yetu hakika, rabuka anazo data
Ukweli utafichuka, majuto hatutahata
Wasaliti wa dunia, binadamu usiwaamini

Moyoni nitafurahi, ukweli ukifichuka
Hakimu nitamsihi, maovu kuyaanika
Njia safi na sahihi, mie tatoa sadaka
Wasaliti wa dunia, binadamu usiwaamini

Msamaha ni wa Baba, moyoni nimewaachia
Sabini Mara saba, hivyo yasema bibilia
Kwa ukweli si haiba, mapenzi tawafichia
Wasaliti wa dunia, binadamu usiwaamini

Tisa beti nafikia, Koffi meshasimulia
Nisitamani kurudia, natumai wamesikia
Haya yote ya dunia, ya mbingu twaazimia
Wasaliti wa dunia, binadamu usiwaamini

© Koffi Brian

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *