Nyumba ya Udongo

Leo mwenyewe natubu, imeshanishinda fani,
Aula nitoe gubu, li’lo mwangu fuadini,
Msambe nawajaribu, nalonga pasi utani,
Miye nyumba ya udongo, vishindo vyazidi kani.

Nikizipiga hesabu, nimefanya kitu gani,
Bado nakosa jawabu, naona sina thamani,
Nawa’chia mashababu, wajigambe hadharani,
Miye nyumba ya udongo, vishindo vyazidi kani.

Heri nipate dhehebu, nikawe mfia dini,
Nizitafute thawabu, zake yeye Mkawini,
Huenda sitawa bubu, humo ndani injilini
Miye nyumba ya udongo, vishindo vyazidi kani.

Narudi sasa kwa babu, nikakae nae tini,
Anipe japo majibu, nishughulike na nini,
Ama niuze kababu, huenda naweza wini,
Miye nyumba ya udongo, vishindo vyazidi kani.

Jama nipeni tabibu, anijuze kwa undani,
Awezaye kunitibu, nami nikawa fanani,
Ila kwa sasa ni tabu, fani bado mtihani,
Miye nyumba ya udongo, vishindo vyazidi kani.

Kipaji kumbe nasibu, hugawa yeye Manani,
Hata upange irabu, kwa vina nayo mizani,
Ila ya kwake ajabu, hutaweza abadani,
Miye nyumba ya udongo, vishindo vyazidi kani.

Japo kwa aghalabu, hukipati darasani,
Usijawe na ghadhabu, kumlaumu Dayani,
Kinyafu sina sababu, ya kubaki uwanjani,
Miye nyumba ya udongo, vishindo vyazidi kani.

© Kinyafu Marcos
MUUMINI WA KWELI.
Dar es salaaam, Tanzania

Maoni 2

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *