Nachagua Amani

Kuna vingi duniani, vyenye tunu na thamani,
Vyavutia si utani, rahisi kuvitamani,
Ila kwangu vyote duni, pasi amani moyoni,
Taacha vyote lakini, nikachague amani.

Doa kingia hubani, sitojifanya rubani,
Nitajibanza pembeni, na niache usukani,
Sijetoneshwa dondani, nichubuke mtimani,
Taacha vyote lakini, nikachague amani.

Madola sitothamini, nikalifike moyoni,
Utu wangu nathamini, nijapo lala bandani,
Katu sitoona soni, hapo ndo kwangu nyumbani,
Taacha vyote lakini, nikachague amani.

Kama kazi ndo kiini, kuwakeketa maini,
Kunendea chinichini, kisisimizi wendani,
Endeleni wafitini, Mola sio athumani,
Taacha vyote lakini, nikachague amani.

Chakulacho we nihini, nijilie vya pipani,
Vijapooza kwa ndani, shibe mie tapateni,
Nikiwa nayo amani, ndani yangu mtimani,
Taacha vyote lakini, nikachague amani.

Ninatua kwa mizani, yote meweka mezani,
Amani ni ya thamani, wazalendo pulikeni,
Koteni ihubirini, amani ya mtimani,
Taacha vyote lakini, nikachague amani.

© Bonface Wafula
(Mwana Wa Tina)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *