Ishi ya Leo na Sasa

Dhamira naazimia, habari nawapeni,
Unyakuzi mewadia, sauti toka mbinguni,
Malaika wasifia, naima tele sikizeni,
Mwisho wako tegemea, Ishi ya Leo na sasa.

Sifungwe na mawazo, kashindwa jitambua,
Wasikufanye gogo, kusudi jiamulia,
Maisha kuyajenga, wasena kitazamia,
Mwisho wako tegemea, Ishi ya Leo na sasa.

Kujiamini hakika, nafsi yako kulinda,
Kujikubali haraka, heshima itapanda,
Kwake baba rabuka, maishani utapenda,
Mwisho wako tegemea, ishi ya Leo na sasa.

Kusema hawatakoma, aila yao chiriku,
Wima ndugu tasimama, matendo safi usiku,
Mtimani jaza neema, hekaluni sio kitu,
Mwisho wako tegemea, Ishi ya Leo na sasa.

Siku hiyo itafika, hukumu itaafikiwa,
Mikaeli malaika, tasimama kwa bwawa,
Mengi kwetu ni mashaka, mienendo usosawa,
Mwisho wako tegemea, Ishi ya Leo na sasa.

Mikaeli tasimama, ye jemadari mkuu,
Kitabu cha uzima, ni samani yake huu,
Walojawa na neema, itakuwa sikukuu,
Mwisho wako tegemea, ishi ya Leo na sasa.

Kimya sitiri nafsi, mlinzi wa heshima,
Kelele ya kuishi, utovu wa hekima,
Dharau ya mahashishi, lanyima mtu uzima,
Mwisho wako tegemea, Ishi ya Leo na sasa.

Mengi Leo tayasema, moyoni kajililia,
Mbinguni si haima, mwenzio tavumilia,
Makosa ya mapema, si kama pundamilia,
Mwisho wako tegemea, Ishi ya Leo na sasa.

Tamati nimefikia, siku hiyo itafika,
Hakuna ajuaye saa, Isa pia malaika,
Sote twasubiria, ujio wa baba Rabuka,
Mwisho wako tegemea, ishi ya Leo na sasa.

© Koffi Brian

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *