Kupata Sio Idili

Naomba niseme wazi, kwetu na liwe bayana,
Mja nataka maizi, unielewe kwa kina,
Ili tusiwe wajuzi, na Mola tukakosana,
Kupata sio idili, ni kudura za Rabana.

Ajabu ya siku hizi, watu izara hawana,
Wamfedhehi Mwenyezi, tena dhahiri mchana,
Limeshakuwa tatizi, wengi linawatafuna,
Kupata sio idili, ni kudura za Rabana.

Huu wangu uchunguzi, kwingi umefanyikana,
Nimeona waziwazi, mambo yakitendekana,
Eti wanazika mbuzi, si kumwomba Maulana,
Kupata sio idili, ni kudura za Rabana.

Haya kweli machukizi, hivi tunavyotendana,
Twatabana kwa henezi, ndulele twachomeana,
Waama ni upuuzi, hivi tunavyofanyana,
Kupata sio idili, ni kudura za Rabana.

Hata tufunge hirizi, na chale tukachanjana,
Tukazivunja za nazi, na dawa tukapakana,
Bure tunajipa kazi, tena twavuta laana,
Kupata sio idili, ni kudura za Rabana.

Huu uwe ufumbuzi, wazazi na nyinyi wana,
Msiifanye ajizi, kusogea kwa Rabana,
Msije pata banguzi, mkabaki farakana,
Kupata sio idili, ni kudura za Rabana.

© Kinyafu Marcos
Chuo cha usimazi wa fedha,
Dar es Salaam, Tanzania.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *