Wajanja Hatari

Imezuka sarakasi, tumeona paruwanja,
Wanakulana mafisi, walojidhani wajanja,
Kwa vijembe na matusi,wenyewe wanajichanja,
Hicho kilimo mahindi, kitawatoka puani.

Wanajitia najisi, nchi ikishuhudia,
Tena ni kadamnasi, shutuma tunasikia,
Wanataka yao kesi, sisi kuwaamulia,
Ahaa!Wakiritimba, mara hii mutaona.

Mbona imetoka hisi, mukawa mahayawani?
Hamutathamini sisi, tuumiao kondeni,
Kuchao munatughasi, munapohodhi mapeni,
Ule ulafi wa fisi, mwishowe ulimponza.

Ninawachia kudusi, mlifi wa deni langu,
Hawakabili waasi, walaji wa jasho langu,
Uje upepo wa kusi, uwatoe nchi yangu,
Sikubali asilani, kila siku kuibiwa.

© Moses Chesire
(Sumu Ya waridi) Kitale

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *