Kikulacho Ki Nguoni

Wawapi mahayawani, wale tulowaamini,
Ola wanavyotuhini, sisi tulomasikini,
Tuliwatia moyoni,tukidhani ikhiwani,
Nimekiri ya wahenga, kikulacho ki nguoni.

Tulipewa pembejeo, na serikali tukufu,
Wakavitumia vyeo, na njia zilizo rafu,
Kwa mitindo ya kileo, wakagawa tukishufu,
Nimekiri ya wahenga, kikulacho ki nguoni.

Huvuna anayepanda, zao likiwa tayari,
Kwa henezi huyatunda, yale yaliyonawiri,
Lakini langu mgunda, ulitima umekithiri,
Nimekiri ya wahenga, kikulacho ki nguoni.

Ninauza kwa hasara, mazao niliyopanda,
Katu sipati tijara, kutoka wangu mgunda,
Wanaowanda ni vyura, mashetani na manunda,
Nimekiri ya wahenga, kikulacho ki nguoni.

Hapa naomba kutua, nisije nikakufuru,
Nyendo zenu nimejua, enyi wakwepa ushuru,
Zitawatoka kwa pua, mukizidi kukusuru,
Nimekiri ya wahenga, kikulacho ki nguoni.

Moses Chesire
Sumu ya waridi
Kitale

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *