Salamu kwa Watajika

Nawaomba wasanifu, wajuzi wa hii kunga,
Nifunzeni ubunifu, nami niitwe malenga,
Nipange beti kwa safu, niwache kuunga unga,
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

Wamalenga maarufu, nyie mulio vipanga,
Miye ni bado dhaifu, kuna jambo lanizonga,
Natafuta wabunifu, wasotumia manyanga,
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

Mtimani nina hofu, hili dhahiri nalonga,
Ningali bado hawafu, sioni pa kujikinga,
Ninawaza maradufu, vipi naweza jiganga?
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

Si kwamba ninakashifu, hilo bayana napinga,
Nonapo wangu uchafu, matozi yalengalenga,
Lini nitafua dafu, niwe na miye kipanga?
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

Sikieni wasanifu, Bumbuji hadi Msanga,
Nipeni ukamilifu, nami nilicheze vanga,
Sijamaliza arifu, bado ni mwana mchanga,
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

Nudhumu isiwe ndefu, kaditama naifunga,
Kumradhi watukufu, pale nilipo bananga,
Sikupanga cheza rafu, nisije shikiwa panga,
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

© Kinyafu Marcos
Dar es salaam, Tanzania.

Maoni 2

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *