Nifunzeni Ubunifu

Nawaomba wasanifu, wajuzi wa hii kunga
Nifunzeni ubunifu, nami niitwe malenga
Nipange beti kwa safu, niwache kuunga unga
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

Wamalenga maarufu, nyie mulio vipanga
Miye ni bado dhaifu, kuna jambo lanizonga
Natafuta wabunifu, wasotumia manyanga
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

Mtimani nina hofu, hili dhahiri nalonga
Ningali bado hawafu, sioni pa kujikinga
Ninawaza maradufu, vipi naweza jiganga?
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

Sikwamba ninakashifu, hilo bayana napinga
Nonapo wangu uchafu, matozi yalengalenga
Lini nitafua dafu, niwe na miye kipanga?
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

Sikieni wasanifu, Bumbuji hadi Msanga
Nipeni ukamilifu, nami nilicheze vanga
Sijamaliza arifu, bado ni mwana mchanga
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

Nudhumu isiwe ndefu, kaditama naifunga
Kumradhi watukufu, pale nilipo bananga
Sikupanga cheza rafu, nisije shikiwa panga
Wajuzi wa hii kunga, nifunzeni ubunifu.

© Kinyafu Marcos
Dar es salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *