Nitunge Nini?

Nawaza nini nitunge, waungwana nijuzeni
Ati miye nikipange, kwayo vina na mizani
Nyoyo zenu kiwakonge, mfurahi mitimani
Niambiyeni magunge, wajuzi wa hii fani.

Mawazo ninayo tele, niwazayo akilini
Naviwaza visakale, na hekaya za zamani
Utata unifikile, sijui nitunge nini
Aheri niwe mpole, kalamu nitue tini.

Nachelea kubananga, nikachekwa hadharani
Nisije umwaga unga, njaa ikaja nyumbani
Nishinde nikipuyanga, nikalala taabani
Waama miye nalonga, leo situngi jamani

Ijapo kweli mkiwa, sina raha asilani
Nikitazama yakuwa, sijuwi nitunge nini
Matozi tele najawa, raha sina fuadini
Kama gunia la chawa, nilibebile kitwani

Kaditamati nafunga, ingawa nina huzuni
Sikwamba miye naringa, waja kweli eleweni
Hofu yangu kuboronga, miye nisiye fanani
Nasubiri umalenga, nipewe naye Manani

© Kinyafu Marcos
Dar es salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *