Wachinjaji

Wachinjaji muchinjao, nyiye wamachinjioni,
munipavyo mshangao, muchinjiapo gizani,
hadi muone machweo, ndipo mungine kazini,
Nipani ufafanuo, ni kitiba ama nini?

Kiza kiwe kimetanda, cha usiku wa manane,
Ndipo mupate mawanda, zizini mukimbizane,
Kwa nini hivyo mwatenda, ama musionekane?
Hebu nipani ukanda, siniache nisonone.

Enyi wa Kisakasaka, Mwera na Mfenesini,
Mnijuvye kwa haraka, siri ya machinjioni,
Kama mila na silika, tijaraye jambo gani?
Jibu lenu nalitaka, ngombe kuchinja gizani.

Ole Kianga na Wete, sogeeni tunongone,
Jibu lenu mulilete, kusudi tuelewane,
kifuani nna tete, semeni nami nipone,
hebu njoni tutete, nawaruhusu munene.

Wadonge Muwanda pia, nanyi nawaulizeni,
jawabu nalingojea, haraka nifisiaeni,
Ni ipi hasa fatua, ngombe kuchinja gizani?
Semeni nipate jua, nitulie fuadini.

Wesha nako Mkoani, nanyi tusikimbiane,
kwanini iwe gizani, tena liwe giza nene?
Ndipo mwende chinjioni, tochi mumurikiane,
kwa nini iwe gizani? naomba tufahamishane.

Kinyasini na Mahonda, nishaingia njiani,
Kidoti nako takwenda, siri kuipekesheni,
Jibu halitawashinda, sababu nawaamini,
Tongoani kwa mawanda, munitoe mashakani.

Meli tano Michewezi, hebu nanyi tuonane,
Hivi sababu ni nini? usiku ndo muzingane,
Mungie vyenu zizini, kwa shime muhimizane,
Iwe usiku kwa nini? mwachinja tuelezane.

Nawaaga ninauka, jawabu nipatieni,
nisijepata gharika, hageuka majununi,
nawapia taridhika, nawaomba nijibuni,
Ipi sababu hakika, ngombe kuchinja gizani?

© Ali Mohammed (Almar)
Kisauni, Zanzibar

Maoni 7

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *