Mapenzi ni Sumu

Penzi halina mwalimu, japo linayo mazao,
Wengi husema li tamu, sijaona ufaao,
Naeleza kwa nudhumu, lisomwe kila uchao,
Mapenzi kweli ni sumu, hudhuru wapendanao!

Penzi linayo misimu, si kila siku kikao,
Bora anayejikimu, si kwa yahe watangao,
Huenda liwe haramu, kwa wadogo wapatwao,
Mapenzi kweli ni sumu, hudhuru wapendanao!

Penzi linao ugumu, barani hadi mwambao,
Hata useme Kiamu, ama kile Kimgao,
Hushinikiza hamumu, ikuleteayo zao,
Mapenzi kweli ni sumu, hudhuru wapendanao!

Penzi lina nyingi hamu, wawili waandaao,
Hakosi kujilaumu, kwao wajiingizao,
Halikosi la hukumu, muda mfupi ujao,
Mapenzi kweli ni sumu, hudhuru wapendanao!

Penzi ni kujiheshimu, wendako na kwa makao,
Mwengine usidhulumu, kwake wewe uwe ungao,
Mkiishika hatamu, wangali watazamao,
Mapenzi kweli ni sumu, hudhuru wapendanao!

Penzi lina majukumu, hufaulu wajuao,
Kila mpenzi awamu, penzi lipate mgao,
Tena si kwa darahimu, kama kwa watesekao,
Mapenzi kweli ni sumu, hudhuru wapendanao!

Penzi huleta wazimu, maovu wayafanyao,
Hekima huwa adimu, mwongozo wakataao,
Watakiwa ukarimu, wawili wajuanao,
Mapenzi kweli ni sumu, hudhuru wapendanao!

© Kĩmani Wa Mbogo (Mwanagenzi Mtafiti)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *