Umekosea Omba Msamaha

Umekosa kuongea, neno lisositahili,
Inna umeshakosea, kusema mengi batili,
Kaanza kuchukulia, yale yanositahili,
Msamaha uuombe, koma kukuli hujali.

Umekosea kucheka, waja wengi kulihali,
Mtu anapoteseka, ni bashasha ukikuli,
Fukara unawacheka, pamoja na atifali,
Msamaha uuombe, koma kukuli hujali.

Umekosea kukana, nasaha bila kujali,
Wazee ukatukana, mashauri ukabali,
Nao wameshakuona, majuto hayako mbali,
Msamaha uuombe, koma kukuli hujali.

Umekosea kusema, umekuwa baradhuli,
Kwake abu na kwa mama, huna heri bilikuli,
Ni bora staha waama, kwa maneno na fiili,
Msamaha uuombe, koma kukuli hujali.

Umekosea kuiba, cha mwenza bila kibali,
Ikiwa hutaki haba, mali yatoka Jalali,
Ukikithiri kuiba, ininasi kujamili,
Msamaha uuombe, koma kukuli hujali.

© Bett Vincent

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *