Kama Wataka Kuoa

Kama wataka kuoa, tumia akili nyingi,
Kaa ukifikiria, hili jambo la msingi,
Ukija jiamulia, uwe tayari na mengi,
Kama wataka kuoa…

Kama wataka kuoa, kwa pupa usiendee,
Huu wangu usia, makini utiliee,
Ndoa chama sikia, usije jililiee,
Kama wataka kuoa…

Kama wataka kuoa, angalia maadili,
Mke mwenye kupoa, aliyetulia tuli,
Atajenga familia, zuri iliyo kamili,
Kama wataka kuoa…

Kama wataka kuoa, angalia yake dini,
Mke aliyejizoa, kwa hulka hurulaini,
Kwa shari takuongoa, akulete peponi,
Kama wataka kuoa….

Kama wataka kuoa, mchague kimavazi,
Mke anayejitambua, kiupande wa malezi,
Hatawahi kuletea, aibu mbele ya wazazi,
Kama wataka kuoa….

Kama wataka kuoa, tafuta anayejituma,
Mke asokutegemea, anajua kuzichuma,
Jamii taendelea, kiuchumi hamko nyuma,
Kama wataka kuoa…..

Kama wataka kuoa, chagua mwenye heshima,
Ndoa kusitiri doa, mke mwenye hekima,
Watoto atawalea, kwa mwenendo ulo mwema,
Kama wataka kuoa….

Kama wataka kuoa, vigezo nishakupa,
Usije ukajutia, kwa kuwa na nyingi pupa,
Ndoa yataka somea, ili sije kula kapa,
Kama wataka kuoa

© Athuman juma

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *