Apewe yake Heshima

Mwendani,
Mama atabaki mama, hadi siku ya kiyama
Mola kampa huruma, na kubwa yake hishima
Hata kama hakusoma, haipaswi kumsema

Mwendani,
Mwanamke mwanamke, Mungu kampa nafasi
Kampa uwezo wake, aweze tulea sisi
Hapigwipigwi mateke, kumuona kama fisi

Mwendani,
Banati huyu banati, ndio pambo la ghulamu
Umpe pendo la dhati, duniya aone tamu
Sio mengi mashariti, na kumkosa nidhamu

Mwendani,
Ajuza huyu ajuza, wengine twamwita nyanya
Usije kumpuuza, pale anapokuonya
Kweli utajiapiza, siku ukija msonya

Mwendani,
Shangazi huyu shangazi, nae huyo ni babayo
Yatii yake malezi, na yote akwambiayo
Haya nakwambia wazi, msikie asemayo

Mwendani,
Narudia huyu Nina, msimdharau kattu
Yatii anayonena, kubisha usithubutu
Miye sielezi tena, kwaheri narudi kwetu.

Mtunzi:Kinyafu Marko
Muumini wa kweli

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *