Machozi ya Fanaka

Kulea mimba si kazi, kazi kumlea mwana,
Shukrani enyi wazazi, kufokea wenu mwana,
Kunilea kwa mbawazi, ninawashukuru sana,
Kuficha tena siwezi, ni machozi ya fanaka.

Kugea staha siwezi, dira yangu ni adabu,
Kukuli kweli azizi, pasi nayo ni taabu,
Heko waliomaizi, kwanziya nina na abu,
Kuficha tena siwezi, ni machozi ya fanaka.

Elimu pia azizi, kunifungua fikira,
Viwango vyote ja ngazi, kwa sasa nina busara,
Nashukuru kwa ghawazi, sare na hata kudura,
Kuficha tena siwezi, ni machozi ya fanaka.

Shukrani wasaidizi, sitosahau ninene,
Kunifanya kuwa ghazi, nyumbani au kwingine,
Kunipa yawe mavazi, mashauri na mengine,
Kuficha tena siwezi, ni machozi ya fanaka.

Kazi sikuli siwezi, mie kufunzwa kwa dhati,
Shukrani kwa wasaidizi, na zingine kujisatiti,
Si siri nasema wazi, furaha kuwa thabiti,
Kuficha tena siwezi, ni machozi ya fanaka.

Kusema kweli ni wazi, kuwa umoja ni nguvu,
Kwishi bila ubazazi, waja hutiyana nguvu,
Na kuhusu rai hizi, zimenitoa uvivu,
Kuficha tena siwezi, ni machozi ya fanaka.

Uvumilivu namazi, wajuzi kunishauri,
Magumu bila ghawazi, ku’mbiwa nitie ari,
Mazuri sasa ni wazi, tena maisha safari,
Kuficha tena siwezi, ni machozi ya fanaka.

© Vincent Bett

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *