Mwana Siti

Tabasamu lako jema, kuliko chochote kile,
Wajulikana kwa wema, utendao huku kule,
Matendo yako ni mema, wasifiwa tangu kale,
Msiti takulinda, takutunza sawa sawa.

Chochote ukitendacho, watenda kwa ufasaha,
Kiwe hiki ama hicho, matokeo ni furaha,
Lawahenga chambilecho, katu huwa sikaraha,
Msiti takulinda, takutunza sawa sawa.

Hata unapokosewa, huonyeshi hamaki,
Utaficha ulotendewa, tadhani kawa haki,
Licha yako kuzomewa, mema huweki bureki,
Msiti takulinda, takutunza sawa sawa.

Furaha umezidisha, penzilo limekolea,
Mengi umeyawezesha, ushauri kanipea,
Mazuri hujakomesha, wazidi kunitendea,
Msiti takulinda, takutunza sawa sawa.

Tano nafunga shairi, ndipo pangu kituoni,
Mimi taleta mahari, na hiyo ndiyo shukrani,
Mola atupe umuri, tufurahi duniani,
Msiti takulinda, takutunza sawa sawa.

© Kiambi Daniel
Mombasa Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *