Nakula kwa Macho

Nawapigiya kayamba, kwa sauti wastani,
Mwenzenu naimba imba, nikiwa huku pembeni,
Na leo sina Kilemba, wala mambo hamsini,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Mwili wangu kama mamba, makunyanzi ya mwilini,
Kitambo siku za rumba, hungenitowa dansini,
Na hata kuruka kamba, nilikuwa namba wani,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Nakumbuka huko pemba, tulikaa baharini,
Hatungevaa mitumba, tuendapo harusini,
Tena hata kujipamba, tulishindana jamani,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Leo misuli mituma, nguvu zake wastani,
Kutembea ninayumba, nayumba yumba njiani,
Uzee ushani ramba, ushaningiya mwilini,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Wasichana wenye namba, niliwafurahisheni,
Kila siku kujigamba, nilipata afueni,
Niliwachezesha rumba, kuzeeka sikudhani,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Japo nina tamba tamba, si kama hapo zamani,
Hata kuicheza rumba, ni hapo kwangu chumbani,
Leo mavazi mitumba, mapya ninunue lini?
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Vijana mnao tamba, mlo na nguvu mwilini,
Muda wenu kujigamba, upo ni leo jamani,
Leo yenu ina bamba, kesho yenu ni usoni,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Nahitimisha kurumba, ‘rangile’ nina amani,
Ninaitamani rumba, naangalia kwa mboni,
Roho safi kama pamba, mie sina walakini
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

© Joel Mburia

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *