Mwanamke Msungo

Wenzangu nyie malenga, heko mno kwa usanii,
Mosi jambo lapiga chenga, wazi nalileta kwa jamii,
Kwenye dinga nao Makanga, waulizana kwa ‘tafitii,
Dini ‘tulete kwenye mwanga, Mashehe pasta na Manabii,
Mwanamke msungo, mbona kakwepa unyago?

Mke ‘kiteknologia, umeadhirika sihaba,
Udijitatali ‘wabugia, utadhani nyoka ya shaba,
Kilingeni ‘mejifungia, mwajadili yake swaiba,
Mwajidai wangu Kagia, mchana kutwa haja shiba,
Mwanamke msungo, mbona kakwepa unyago.

‘Toboa pua na sikio, maisha hamjatoboa,
Shahada nazo kimbilio, maadili mema kabomoa,
Usawa mwadai ndio, mume nje naye kamtoa,
‘kimpata kwa jiranio, yagololi wayakondoa,
Mwanamke msungo, mbona kakwepa unyago?

Ukiwalola mitaani, wanatamba kwa motorola,
Beibi jina la mpangoni, kumbe ni mwani wa bakola,
Kila siku walia mwani, mkifizia zetu hela,
‘kikosekana vipochini,dume hili talala jela,
Mwanamke msungo, mbona kakwepa unyago?

Naye huyu mke kwa ndoa, ni ndoa la mkeka nusu,
Kila siku kujipodoa, na jirani kapewa busu,
salamu’ke ni poa poa, mapenzi ng’o hayakuhusu,
Yako mapenzi yamepoa, kwa wenzi wake ni sususu,
Mwanamke msungo, mbona kakwepa unyago?

Mie ‘mefikia ukingo, yote ‘lokuwa akilini,
Na ukimuoa msungo, ‘kupewa gazeti jioni,
yake dawa msungo, makungwi m’wafundisheni,
Kutaneni nyote unyago, wanawake ‘shauriweni,
Mwanamke msungo, mbona kakwepa unyago?

© Daniel Kiambi
Mombasa Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *