Vijana wa Kizazi Kipya

Kweli ujana ni moshi, vijana msikieni,
Wavulana kwa magashi, kizazi hiki kizani,
salimini ili twishi, lazima tuwe makini,
Kizazi hiki kizazi, mwenda pole hajikwai.

Vijana walaumiwa, wema hawazingatio,
Nasaha wanapopewa, ja nyama kwenye kioo,
Kuongea yaso sawa, wafanyayo machukio,
Kizazi hiki kizazi, mwenda pole hajikwai.

Vijana siku hizi, matendo yao aibu,
Kuyaacha hawawezi, mazoea kuwa tabu,
Ujanja kwao ni wazi, vya watu wanaghusubu,
Kizazi hiki kizazi, mwenda pole hajikwai.

Kizazi hiki cha nuksi, vijana sasa kinyume,
Mama kupata matusi, abu ngumi aandame,
Nasema kwa kuhisi, haya mabaya mukome,
Kizazi hiki kizazi, mwenda pole hajikwai.

Ba’dhi wakana masomo, eti hayana maana,
Wengine huhepa kimo, na miaka kuachana,
Elimu h’ina kipimo, usoni mwako maana,
Kizazi hiki kizazi, mwenda pole hajikwai.

Ghulamu vazi labwaya, binti mwili hadharani,
Ajabu twafurahiya, tunaenda hatarini,
Tuache hya mabaya, nakuli toka moyoni,
Kizazi hiki kizazi, mwenda pole hajikwai.

Kizazi hiki chatisha, vijana nao hutisha,
Pombe na sigara tosha, ndoto zao zimeisha,
Na mapenzi ovyo kisha, sheni eti raha tosha,
Kizazi hiki kizazi, mwenda pole hajikwai.

© Vincent Bett

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *