Mpatie Mamangu Amani

Mwanawe fasiti boni,sina furaha moyoni,
Niyaonayo jamani,hayanipi mi amani,
Sijui kakosa nini,humuhumu duniani,
Mamangu adhulumiwa,nanyi babu mwangalia,

Hana kweli pa kulima, baba shamba kakodesha,
Huu kweli siyo wema,bali yanihuzunisha,
Nikijaribu kusema,inanipanda puresha,
Zindukeni jomba zangu,mumwokoe mama yangu,

Acheni kuangalia,mamangu akiteseka,
Hana furaha kwa ndoa, nisikizeni hakika,
Yale anayapitia, ukweli si ya kucheka,
Kwa mkuu wa ukoo,nakuomba muokoe,

Ami zangu na shangazi, sijifanye hamuoni,
Haya mambo mwamaizi,toka nje hadi ndani,
Babangu kama mzazi,ananikera jamani,
Haya mambo afanyayo,mwanawe sifurahishwi,

Nyanya mkopoa abu,iweje unanyamaza?
Mjukuu nina tabu, maswali najiuliza,
Kila kucha masaibu, ukweli yaniumiza,
Zinduka ewe nyanyangu, mamangu apate haki,

Hosea Namachanja
“Chozi la Kunguni”
Bungoma, Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *