Nyani Haoni Mandole

Ingekuwa ni kuona, nyani angeona vile
Machoye yangaliona, nae kumbe walewale
Kamwe asingeliguna, ana mando kama lile
Nyani haoni mandole

Kamwe sijione mwema, eti umefanya yale
Kwa kipi umejipima, uone u mteule
Hiyo kazi ya Karima, muumbaji maumbile
Nyani haoni mandole

Maisha yana vilima, kushuka na tambarale
Kukwazana ni lazima, mloishi toka pale
Si vyema kujitakama, kujiona ndio vile
Nyani haoni mandole

Vipi ujione bora, kwa yale uyatendile
Na mwingine hana fora, imekukosa simile
Unakiliza king’ora, mara hivi mara vile
Nyani haoni mandole

Salamu ni kago jema, walotukaga wakale
Ni agizo la Karima, ukilifanya tawile
Lakini ukitunyima, ni kosa ulitendile
Nyani haoni mandole

Ukimnanga Kijoka, kwa maneno ya mshale
Zitaondoka baraka, ulizojaliwa tele
Huwezi kufaidika, hata uishi milele
Nyani haoni mandole

Hakuna mkamilifu, watu wote tupo vile
Mengine udanganyifu, kama mpira na Pele
Kiumbe usahulifu, kamwe usikutawale
Nyani haoni mandole

© Hamisi A.S. Kissamvu
Mabibo, Dar es Salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *