Kuthubutu

Uoga wa kuthubutu, ni ngumu kwako kujua
Daima hubaki butu, pasi mapya kugundua
Tabakiwa na kutu, haishi kwa kusugua
Ukitamani kujua, ni vema ukathubutu

Uoga wa kuthubutu, ni nguzo iloungua
Haitosimama katu, ni nyepesi kama bua
Haifai kila kitu, na hata kwa kupaua
Ukitamani kujua, ni vema ukathubutu

Uoga wa kuthubutu, vingi huwezi tambua
Dawamu huoni katu, ni meli au mashua
Huofia kuthubutu, bila kutaka kujua
Ukitamani kujua, ni vema ukathubutu

Uoga wa kuthubutu, ni sumu inayoua
Usilambe mwanakwetu, kago utalikagua
Utenge ja samawatu, umbali ulivyokua
Ukitamani kujua, ni vema ukathubutu

Uoga wa kuthubutu, ni bomu la kutegua
Litaua kila mtu, kama hatuta tegua
Anuari ni kiatu, kanyaga uso pajua
Ukitamani kujua, ni vema ukathubutu

Uoga wa kuthubutu, ni donda tunaugua
Tunaenda matumatu, machungu yatusumbua
Tusihofu kuthubutu, ndio tiba nayojua
Ukitamani kujua, ni vema ukathubutu

Uoga wa kuthubutu, kitendawili tegua
Ametega Mola wetu, ambae anatujua
Tuondoe hofu zetu, tunapotaka ng’amua
Ukitamani kujua, ni vema ukathubutu

Uoga wa kuthubutu, ni vyema ukatambua
Tusihofu kuthubutu, kujaribu jinasua
Rabi ndio nguzo yetu, mlinzi kila hatua
Ukitamani kujua, ni vema ukathubutu

Uoga wa kuthubutu, ni janga litatuua
Tusipolikana katu, hatutopiga hatua
Tuondoe hofu zetu, mipango iwe murua
Ukitamani kujua, ni vema ukathubutu

Uoga wa kuthubutu, tamati sasa natua
Tupo kati ya msitu, najua halijatua
Tuufanye uthubutu, tuweze piga hatua
Ukitamani kujua, ni vema ukathubutu

© Hamisi A.S. Kissamvu
Dar es Salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *