Chungu na Pegiko

Kutegemea pegiko, ndio tabia ya chungu
Kisipate hangaiko, kikaja tenguka tengu
Kama mwana na mbeleko, huwezi engua engu
Mambo huenda mtengu, chungu pasi na pegiko

Chungu pasi na pegiko, itakufika mizungu
Utapata hangaiko, huwezi kuvuga dengu
Adha yake mnenguko, kila muda nengunengu
Mambo huenda mtengu, chungu pasi na pegiko

Chungu pasi na pegiko, ni duni usoni mwangu
Inanipa hamaniko, mnani watu wa tangu!
Kama pegiko haiko, chombo kitakwenda tengu
Mambo huenda mtengu, chungu pasi na pegiko

Chungu pasi na pegiko, tuvitenge viwe tengu
Mpishi wa hadhi yako, kiepuke hiki chungu
Kikae mbali na kwako, kina madhila mwenzangu
Mambo huenda mtengu, chungu pasi na pegiko

Chungu pasi na pegiko, ni donda kichwani mwangu
Sijui hapo liliko, huonwa na kono langu
Nahofia mnenguko, vikinenguka machungu
Mambo huenda mtengu, chungu pasi na pegiko

Chungu pasi na pegiko, tamati natia pingu
Pakutegemea hiko, utavunja chako chungu
Hiyo sawa na mbeleko, itachanika mwenzangu
Mambo huenda mtengu, chungu pasi na pegiko

© Hamisi A.S. Kissamvu
Dar es Salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *