Kiswahili Lugha Yetu

Katika zilizo tamu, lugha zenye uthubutu
Kiswahili kiko humu, huwezi kiacha katu
Sasa tukipe hatamu, kivuke mipaka yetu
Kiswahili lugha yetu, tuilinde washairi

Tuilinde washairi, Kiswahili lugha yetu
Tuongeze umahiri, kufunza vizazi vyetu
Misemo ilo mizuri, tusije iacha katu
Kiswahili lugha yetu, tuilinde washairi

Washairi tuilinde, tusikae matumatu
Lugha ivuke mabonde, ifike hadi Karatu
Nawaomba chondechonde, hili tuweze kufutu
Kiswahili lugha yetu, tuilinde washairi

Za ghaibu hazimati, ninaziona ni butu
Ya nini tuzipe hati, tukaibeza ya kwetu
Lugha hii ni yakuti, haishi thamani katu
Kiswahili lugha yetu, tuilinde washairi

Ipewe kipaumbele, katika mashule yetu
Masomo yafunzwe vile, kwa lugha hii ya kwetu
Hapo kitasongambele, hiki Kiswahili chetu
Kiswahili lugha yetu, tuilinde washairi

Hakuna kilicho chema, zaidi ya chake mtu
Waliyasema wa zama, siwezi tengua katu
Kiswahili lugha njema, haikubakisha kitu
Kiswahili lugha yetu, tuilinde washairi

Tukikuze Kiswahili, kupitia tungo zetu
Tendi na vitendawili, viwe mafunzo kwa watu
Tuache lugha za mbali, kufundishia wanetu
Kiswahili lugha yetu, tuilinde washairi

Tamati ya Kiswahili, kina ncha sio butu
Cha penya kila mahali, wala hakipatwi kutu
Kisitiwe idhilali, kikatenga vinywa vyetu
Kiswahili lugha yetu, tukilinde washairi

© Hamisi A.S. Kissamvu
Dar es Salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *