Ugenini

Ukishafunga safari, ya maisha kujaribu
Kwenda itafuta heri, kuelekea janibu
Nyumbani ukahajiri, ukaisha ughaibu
Ugenini kuna tabu, sio sawa na nyumbani

Sio sawa na nyumbani, ni mengi yatakusibu
Na yote huwa mageni, mengine ya kughilibu
Huipata hali gani, ukaitika taibu
Ugenini kuna tabu, sio sawa na nyumbani

Kwa hili halina kani, ni jambo la aghalabu
Unakua mashakani, hakishi kisebusebu
Kuwa mbali na nyumbani, haliyo huwa ya bubu
Ugenini kuna tabu, sio sawa na nyumbani

Nyondenyonde haziishi, ja simba aso sharubu
Ukaapo hapatoshi, huwaoni maswahibu
Huwezi kuwa mcheshi, kila kitu huwa tabu
Ugenini kuna tabu, sio sawa na nyumbani

Umezoea ugali, mlo unaouhibu
Leo uko nao mbali, kwa vile uko ghaibu
Kachumbari pamwe wali, kuvipata ni nasibu
Ugenini kuna tabu, sio sawa na nyumbani

Sio sawa na nyumbani, yaoneni maajabu
Msambe ni kisirani, kwa haya nilohutubu
Maisha ya ugenini, kwangu naona adhabu
Ugenini kuna tabu, sio sawa na nyumbani

Japo upate thumni, kutanzua madhurubu
Bado haina thamani, kwa vile upo janibu
Ungalikuwa nyumbani, ingefutu matilabu
Ugenini kuna tabu, sio sawa na nyumbani

Kaditama nimefika, nahodha wa marikebu
Ugenini ni mashaka, sikai nipate tabu
Nanga nimeshaitweka, pahala pa wangu babu
Ugenini kuna tabu, sio sawa na nyumbani

© Hamisi A.S. Kissamvu
Dar es Salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *