Adabu Niandame

Adabu nielekeze, nikuli yanostahili,
Tasfida niendeleze, pia ninene ukweli,
Katu mema nieneze, na hata kwa atifali,
Staha abadi nikuze, nikome yasostahili.

Nikome yasostahili, nataka matendo bora,
Heshima unibadili, nifanye kuwa imara,
Machukio yawe mbali, niandisi njia bora,
Nikanywapo nikubali, rai zisiwe hasara.

Rai siziwe hasara, nizivae za heshima,
Nivaazo kila mara, ziwe za mfano mwema,
Nisikie ya busara, kwanziya abu na mama,
Adabu hii imara, uniandame daima.

Uniandame daima, nishiriki na wengine,
Hadhi unifanye mwema, ushiriki nisikane,
Niwe wa kupanga mema, pia kutenda mengine,
‘Siniandisi nadama, unitenge na ubene.

Unitenge na ubene, furaha kutamanika,
Unafiki niachane, ni nidhamu nakutaka,
Uhuni usonekane, nipate kuaminika,
Staha abadi ninene, nisije kusononeka.

© Vincent Bett

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *