Heshima

Heshima kitu kizuri, kokote ulimwenguni,
Heshima kweli fahari, kila pembe duniani,
Basi na iwe desturi, tufaulu dawamuni,
Heshima kweli heshima, niko wima kukusifu.

Heshima kweli si siri, tuonyeshe mileleni,
Sote twataka mazuri, mwetu sisi maishani,
Lakini bila busuri, katu hatuandamani,
Heshima kweli heshima, niko wima kukusifu.

Kila mja ufikiri, vilevile kwa makini,
Kwamba maneno mazuri, ni baraka kulikoni,
Pia vitendo vizuri, tena baraka yakini,
Heshima kweli heshima, niko wima kukusifu.

Heshima ni kama tari, kwa walo uongizini,
Ni wao hutoa amri, tuwafuate nyayoni,
Kwani ni wanakadiri, hufanya ipasavyoni,
Heshima kweli heshima, niko wima kukusifu.

Kukosa staha hatari, kwa wanafunzi shuleni,
Hivyo ni kujiathiri, ni kinyume masomoni,
Kweli na muwe hadhari, mjiebuke tabuni,
Heshima kweli heshima, niko wima kukusifu.

Heshima siyo dosari, itawale majirani,
Kwani kunena dhahiri, ni kiini cha amani,
Tukuli bila aziri, tuondoe taraghani,
Heshima kweli heshima, niko wima kukusifu.

Adabu kama bikari , kwa upande wa fukoni,
Yale yatakayojiri, yote yataja laini,
Staha siyo kitimiri, tutangaze hadharani,
Heshima kweli heshima, niko wima kukusifu.

© Vincent Bett

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *