Mama Niombee Dua

Mama niombee dua, nakuomba kwa hisani
Ahsante kunikopoa, kunileta duniani
Malezi kunipatia, masomo kutonihini
Mama niombee dua.

Mama niombee dua, udumu mwangu moyoni
Niswafiye yako nia, pendo lizidi thamani
Ya kwangu yawe murua, ipunguwe mitihani
Mama niombee dua.

Mama niombee dua, nizikumbuke ihsani
Yote ulonitendea, niyatie akilini
Nisiwahi kukosea, kesho nikenda motoni
Mama niombee dua.

Mama niombee dua, nisimfwate shetwani
Niwe na njema tabia, nizingatie ya dini
Nisiende piapia, kujitia madhambini
Mama niombee dua.

Mama niombee dua, niwe na siha mwilini
Afiya kunikolea, niwe timamu kichwani
Heshima kushikilia, hekima iweko ndani
Mama niombee dua.

Mama niombee dua, nikuhifadhi moyoni
Niwe nakuhudumia, leo hadi uzeeni
Safari ikiwadia, tukutanishwe peponi
Mama niombee dua.

Mama niombee dua, nakupenda niamini
Machozi nakulilia, magoti naweka chini
Shairi namalizia, nimefika ukingoni
Mama niombee dua.

N’nge Mpole
Mshairi Kinda
Suleiman Abdallah Bambaulo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *