Watoto ni Baraka

Washirika nauliza, mlijibu langu swali,
Nisibaki ninawaza, majibu nitakubali,
Vema mkinieleza, niuelewe ukweli,
Unapopata mtoto, ni baraka zake nani?

Mungu ndiye mwenye yote, watoto hukujalia,
Mpe sifa kwa lolote, mengi amekupatia,
Kushukuru usisite, kwa maombi kumwambia,
Unapopata watoto, ni baraka zake Mungu.

Kwa heshima nauliza, mnijibu waziwazi,
Muweze kunieleza, wafanyavyo viongozi,
Jukumu wanaloweza, wanaoitwa wazazi,
Kazi yao kwa watoto, nauliza ndiyo gani?

Msiwachukize wana, watendee yalo mema,
Msitamke laana, waombee dua njema,
Husoma wanavyoona, wakaipata hekima,
Waleeni na maonyo, muwaelekeze vema.

Watu wana njia nyingi, wanavyolea wanao,
Kunayo mawaidha mengi, yaliyopo kama ngao,
Nielezeni kwa wingi, tunahitaji mazao,
Nataka mnieleze, mtalea mwana vipi?

Mwongoze kwa njia njema, kwa Mungu umwelekeze,
Muonyeshe ya heshima, mwana usibembeleze,
Mwelimishe ya hekima, yafaayo umweleze,
Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *